Rais Jakaya Kikwete amesema ana orodha ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara kukwepa kodi kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema anaifanyia kazi orodha hiyo na akishamalizana nayo atamkabidhi Kamishna Mkuu wa TRA, Harry Kitilya, ili achunguze na kuwafukuza kazi wafanyakazi watakaothibitika kujihusisha na vitendo hivyo.
Aliyasema hayo jana wakati akizungumza na viongozi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) na wadau wa bandari Tanzania alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni ufuatiliaji wa agizo alilotoa mwezi uliopita kupunguza msongamano wa makontena.
Alisema serikali haiwezi kuvumilia watu wanaoikosesha mapato.
Akitoa mfano namna wizi huo unavyofanywa, Rais Kikwete alisema wanaweza kuendesha zoezi hilo kwa simu ambapo mtu aliyeko Dubai anapewa maelezo namna atakavyojaza fomu ili mzigo wake usipite kwenye scanner, hali inayoweza kupitisha mizigo haramu kama dawa za kulevya.
Alisema wafanyakazi na wafanyabiashara hao wanatumia udanganyifu kuwa kontena hizo zimebeba mitumba, kumbe ndani ya mitumba hiyo wakati mwingine inatumika kufunika magari.
``Ninayo orodha ndefu na nitaikabidhi kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Kitilya ili awafuatilie na ahakikishe anawatimua kazi mara moja wale watakaobainika wanahusika na mchezo huo ili tuanze upya,`` alisema.
Alisema serikali haiwezi kuvumilia kuwa na wafanyakazi wanaokula njama za kuipotezea mapato.
Kikwete alisema bandarini kuna uzembe mkubwa ambao hauvumiliki na aliuagiza uongozi kuondoa matatizo yaliyopo badala ya kukaa na kunung`unika.
Alisema msongamano wa makontena umekuwa ukiisababishia serikali kukosa mapato mengi na alisisitiza kuwa bandari ni sehemu muhimu ambayo serikali haiwezi kuiacha iwe ya hovyo.
Akiwa katika kitengo cha kuchunguza bidhaa katika kontena, Tiscan, Rais Kikwete alisema maelezo aliyopewa na TPA yanatofautiana na yale aliyopewa na viongozi wa Tiscan.
``Hapa mbona mimi sielewi naomba mnieleweshe, hawa Tiscan wanasema wana uwezo wa kuchunguza hata makontena 200 kwa siku ila wanasema tatizo ni nyinyi hamleti kontena za kutosha... Jamani fanyeni kazi na muachane na visingizio na malalamiko,`` alisema Kikwete.
Aliagiza mamlaka hiyo impe taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa upunguzaji wa makontena ndani ya wiki mbili zijazo na aliahidi kutembelea tena bandari hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Forodha, Otieno Igogo, alimweleza Rais Kikwete kuwa wadau wa Bandari ya Dar es Salaam walikubaliana kulipa dola 30 ikiwa ni gharama za kuhamishia kontena moja katika bandari kavu.
Igogo alimweleza Rais kuwa ingawa wadau wote wamekuwa wakichangia, Kampuni ya Kimataifa ya Kupakua Kontena Bandarini (TICTS), imegoma kutoa fedha hizo.
Alisema dola 30 ambazo TICTS walipaswa kulipa kwa kila kontena linalohamishiwa bandari kavu kama wanavyolipa wadau wengine, zimekuwa zikitolewa na TPA.
Baada ya kauli hiyo ya Igogo, Rais alisema anashangaa kuona jeuri hiyo ya TICTS na kusema kuwa TPA ina mamlaka, lakini haitaki kuyatumia.
Kikwete alisema TPA imefanya vizuri kulipa gharama ambazo TICTS imekataa kuzilipa, lakini aliagiza mamlaka hiyo ihakikishe TICTS inazirudisha mara moja.
``Nyinyi mnashangaza sana, mna mamlaka, lakini hamyatumii... Sasa hizi gharama lazima walipe na wakiwashinda mwelezeni waziri na waziri akishindwa niambieni mimi,`` alisema.
Wakati huo huo, Kikwete alikataa maelezo marefu ambayo Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraem Mgawe, alitaka kuyasoma mbele yake na badala yake akamtaka amweleze sababu za msongamano kutoma lizika.
Baada ya kuelezwa hivyo, Mgawe alimweleza Rais Kikwete kuwa kikosi kazi kilichoundwa kufuatia agizo lake kinaendelea kujitahidi kuondoa msongamano uliopo.
Alisema Mamlaka inatarajia kuwa utekelezaji wa mikakati iliyowekwa itafanikisha kupunguza hali ya msongamano mwezi Machi mwaka huu.
Mgawe alisema katika kipindi cha mwaka 2007/08, TPA ilihudumia tani milioni 6.239, ambalo ni ongezeko la tani 227,222 au asilimia 3.8 ikilinganishwa na tani milioni 6.003 zilizohudumiwa mwaka 2006/07.
Alisema katika kipindi hicho mamlaka ilipata ziada ya Sh. bilioni 37.879 kutokana na mapato ya Sh. bilioni 168.789 na matumizi ya Sh. bilioni 133.909.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar