Obama kufafanua mpango wa kuondoa majeshi, baadae leo
Maafisa wa ngazi za juu katika utawala wa rais Barack Obama wamesema kuwa Marekani itaondoa majeshi yake kutoka Irak hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka 2011.Rais Obama mwenyewe anatarajiwa kufafanua mpango huo baadae leo.
Anatazamiwa kufafanua mpango huo kwenye kambi ya kijeshi iliyopo North Carolina.Marekani kwa sasa ina wanajeshsi laki 1na 42 alfu. Zaidi ya 4,250 wameuawa tokea Marekani iivamie Irak mnamo mwaka 2003.
Obama anatazamiwa baadae leo kuitangaza tarehe 31 ya mwezi agosti mwaka 2010 kuwa siku ya mwisho ya harakati za kijeshi kwa Marekani nchini Irak.Hatahivyo baadhi ya wanachama wa chama chake -Demokratik wameonyesha wasiwasi kwamba mpango wake umechelewa. Obama aliahidi kuondoa majeshi ya Marekani kutoka Irak mnamo muda wa miezi 16 mara baada ya kuingia madarakani.
Rais Obama alikuwa mpinzani wa vita vya Irak tokea Marekani kwa kushirikiana na nchi zingine imvamie Saddam Hussein.Hatahivyo mpango wa rais Obama unalenga shabaha ya kubakiza wanajeshi alfu 50 watakaotoa ushauri kwa majeshi ya Irak na kulinda maslahi ya Marekani nchini humo. Lengo hilo limelaumiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi bibi Nancy Pelosi .Akizungumza katika mahojiano ya televisheni bibi Pelosi amesema haoni sababu ya kuhalalisha idadi hiyo ya askari kuendelea kubakia nchini Irak.Amesema askari kati ya alfu 15 hadi alfu 20 wangelitosheleza.
Rais Obama alikutana kwa faragha na viongozi wa bunge hapo jana ambapo alifahamisha juu ya mpango wa kuondoa majeshi yote ya Marekani kutoka Irak hadi kufikia mwaka 2011.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar