Wachina hao walipanga kufanya maandamano hayo jana kuanzia Uwanja wa Uhuru na kupitia Barabara ya Mandera hadi Makao makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ambako walipanga kutoa tamko lao juu ya mauaji hayo ya Guo Chenwei (25) aliyeuwawa Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa kupigwa risasi shingoni wiki hii.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wafanyabiashara Wachina nchini, Huang Zichan, alisema licha ya kutoridhika na majibu waliyopewa kwa mdomo kutoka makao makuu ya polisi kuwa ulinzi hautakuwepo katika maandamano yao wamelazimika kusitisha hadi siku nyingine watakayoipanga upya.
“Wametueleza kwa mdomo tumewaomba watujibu kwa barua wamesema kesho (Leo) watatuita kutupa jibu kwa maandishi kuwa tusifanye maandamano hayo hadi siku nyingine kwa kuwa askari wengi wameelekezwa kwenye operesheni ya kusaka majambazi maeneo mbalimbali ya jijini,” alisema Zichan.
Zichan alisema wamesikitishwa na hatua hiyo ya kuzuiliwa kufanya maandamano yao hata hivyo, wanasubiri maelezo ya barua ya leo kisha wataandaa maandamano siku nyingine.
“Hili ni tukio la kwanza kutokea tangu tuwe hapa nchini na mauaji haya kama hayatapigiwa kelele yataendelea na kuathiri uchumi wa nchi na kuharibu uwekezaji kwa wageni, kwani tukio hili limesharipotiwa na vituo vikubwa vya habari vya kimataifa ikiwemo China na nchi za Asia, hivyo inaweza kuleta madhara ya uwekezaji hapa Tanzani,” alisema Zichan
Zichan aliongeza maandamano hayo ya amani yalikuwa na lengo la kukemea uovu wote dhidi ya wageni ambao umeonekana kuibuka eneo hilo la Kariakoo.
Awali ilidaiwa Wizara ya Mambo ya Ndani nayo ilipelekewa nakala ya barua ya maandamano hayo, lakini msemaji wa Wizara hiyo, Isaac Natanga alisema hakupokea barua yoyote kutoka kwa wachina inayohusiana na masuala ya maandamano yao.
“Sikupokea barua kuhusu maandamano na jambo hulo si la kwetu ni la polisi, hivyo waulize polisi sisi hatuhusiki na hatukupokea barua ya maandamano,’’ alisema Natanga.
Naye Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam, Suleiman Kova alipotakiwa kueleza juu ya maandamano hayo alisema suala hilo lipo juu ya uwezo wake na kwamba suala hilo limeelekezwa ngazi za juu kwa kuwa inaingilina na ushirikiano wa kimataiafa.
Hata hivyo alipoulizwa msemaji wa Jeshi la polisi, Abdalla Msika kuhusiana na maandamano hayo, alisema yupo nje ya ofisi kwa matibabu na hakuwa na taarifa kuhusiana na maandamano hayo.
Akizungumzaia mazishi na kijana huyo wa kichina, Zichan alisema hatazikwa hadi wazazi wake watakapowasili wiki ijayo kukamilisha taratibu za kusafirisha maiti.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar