Senin, 23 Maret 2009
HOTELI HIZI ZA TANZANIA ZIMETEKETEA KWA MOTO...
Hotel za kitalii za Paradise Holiday Resort na Oceanic Bay and Resort zilizo katika ufukwe wa Bahari ya Hindi wilayani hapa, zimeteketea kwa moto. Moto huo ulioteketeza hoteli zote mbili kwa muda wa saa moja leo, ulianzia jikoni katika Hoteli ya Paradise na kushika mtungi wa gesi na kusambaa kwa kasi kutokana na hoteli hiyo kuezekwa kwa makuti na kuwapo upepo mkali.
Moto ulikuwa ukiwaka kwa juu usawa wa meta 30. Baada ya kuona Hoteli ya Paradise inawaka, wafanyakazi wa hoteli jirani ya Oceanic Bay walikwenda kutoa msaada na wakati wakiendelea kusaidia, ghafla moto ulishika katika hoteli yao na wao kushindwa kurejea kuokoa mali.
Kutokana na moto huo kushika kasi, wageni waliokuwapo walihaha kujiokoa na baadhi yao kufanikiwa kuondoka na mizigo yao. Hata hivyo, hakuna mtu aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha.
Katika Hoteli ya Paradise ambayo ni maarufu kwa mikutano, iliyopo umbali wa takriban kilometa 60 kutoka Dar es Salaam, sehemu ambayo haijaungua ni ya chakula na vibanda vichache ufukweni, wakati Hoteli ya Oceanic sehemu iliyosalia ni baa peke yake.
Katika tukio hilo lililotokea saa 4.30 asubuhi, magari matatu yaliyokuwa katika Hoteli ya Paradise yaliungua, moja aina ya Nissan Patrol namba T382 ASR liliteketea lote na mengine yaliyoungua ni la Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mbeya aina ya Toyota GX namba STK 3240 na Toyota Land Cruiser namba T 182 ATX lililokuwa likitumiwa na Dk. Donath Mrawira.
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo aliyekuwa eneo la tukio, Serenge Mrengo, alisema, “moto umeshika kasi sana kwa sababu ya kuezekwa kwa makuti na upepo mkali, hii ni changamoto kwetu kubadili mtindo wa kuezekea makuti”.
Akielezea jinsi walivyouona moto huo, mkufunzi kutoka Canada aliyekuwa akitoa mafunzo kwa mameneja wa mikoa 21 wa Tanzania bara wa Tanroads, Dk. Donath Mramira, alisema “baada ya kutoka mapumziko ya chai kwenye saa 4.30 asubuhi tukiwa ndani, ghafla umeme ulikatika na tuliamua kuendelea na mafunzo, lakini dada mmoja alifungua mlango tupate hewa ndipo tukaona watu wanalia.
“Tulidhani kuna mtu amekufa, lakini kufuatilia vizuri tukaona hoteli inaungua moto, mimi niliokoa laptop yangu na projekta tu na hili gari lililoungua ni la rafiki yangu aliyeniazima nilitumie nikiwa hapa nchini”. Hata hivyo, Mwenyekiti wa Hoteli ya Paradise ambaye pia ndiye mmiliki wake, Abdullahi Nur Guled, alisema hoteli hiyo imekatiwa bima na thamani yake ni zaidi ya dola milioni 10 za Marekani (sawa na zaidi ya Sh bilioni 13).
“Wasiwasi wangu ni wafanyakazi ambao wako 180 watakosa kazi na serikali itakosa mapato, achilia mbali wale wanaoajiriwa kwa kutuletea vitu hotelini,” alisema. Naye Meneja Uendeshaji wa Paradise, Shukri Ali, alisema hoteli hiyo iliyoanza kutoa huduma mwaka 1997 ilikuwa na uwezo wa kupata faida ya dola 60,000 hadi 80,000 kwa siku kutokana na huduma zake.
Meneja huyo aliyedai hawajafanikiwa kuokoa kitu, alisema hoteli hiyo ina vyumba 82 na wakati tukio linatokea, ilikuwa na wageni 89 waliopanga na watu 70 waliokuwa wakihudhuria mikutano minne tofauti, ukiwamo huo wa Tanroads.
Mkuu wa Wilaya alisema magari ya zimamoto yalitoka Dar es Salaam na wilayani Kibaha na kuongeza: “Sisi Bagamoyo hatuna gari la kuzimia moto, mwaka juzi Halmashauri ililipa zaidi ya Sh milioni 400 lakini hadi leo gari halijafika”.
Magari yaliyoonekana kutoa huduma za kuzima moto huo ni ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam namba STK 1066 na SM 5778. Kwa upande wa Meneja Mkuu wa Hoteli ya Oceanic Bay, Rahul Nayar, alisema hoteli yake ilikuwa imeajiri wafanyakazi 200 na kutokubali kuzungumzia lolote kwa madai mmiliki yuko Dubai.
“Siwezi kuzungumzia hasara, mwenye hoteli yuko Dubai ndiye anayefahamu kila kitu,” alisema. Thamani halisi ya uharibifu haikuweza kupatikana mara moja, kwani hakukuwa na mtu aliyekuwa tayari kuzungumzia hilo leo. Uezekaji makuti umekuwa ukichochea kasi ya moto kama ilivyotokea Septemba 22 mwaka juzi, ambapo Hoteli ya Sea Cliff ya Dar es Salaam ikiwa na vyumba 92 nayo iliungua moto kwa staili kama hii.
Langganan:
Posting Komentar (Atom)
Tidak ada komentar:
Posting Komentar