VURUGU kubwa zimeibuka jana katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na kusababisha Jeshi la Polisi kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kutawanya wanafunzi waliokuwa wakifanya vurugu na kuvunja milango tisa ya majengo ya mabweni na utawala, wakidai kuchelewshewa mikopo.
Tayari wanafunzi watatu ambao wanadaiwa kuwa ni vinara wa mgomo huo wameandikiwa barua za kutimuliwa ambazo watakabidhiwa wakati wowote kuanzia leo, Mwananchi imeelezwa.
Katika mgomo huo ulioandaliwa na kundi la wanafunzi wa kitivo cha elimu wa mwaka wa kwanza katika kundi la pili lilioingia chuoni hapo tangu Januari, ulianza mapema jana muda mfupi kabla ya kuingia madarasani. Wanafunzi hao walianza fujo hizo wakidai kuwa tangu wafike chuoni hapo, hawajapewa fedha zao kutoka Bodi ya Mikopo.
Wanafunzi hao walidai kuwa wamekuwa wakiishi maisha ya tabu na manyanyaso makubwa sana, huku wakisema kuwa wanafunzi wa kike wamekuwa wakilazimika kufanya mapenzi na Wachina wanaosimamia majengo katika chuo hicho ili kupata fedha za kujikimu na kupunguza makali ya maisha.
Waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Kasalali Emmanuel alisema kuwa tatizo kubwa linalotokea katika chuo hicho ni pamoja na baadhi ya watu kutaka umaarufu kupitia katika matatizo ya wanafunzi hao.
Emmanuel alidai kuwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imekuwa ndio tatizo kubwa linalofanya kuwepo na mgomo na akatahadharisha kuwa kama tatizo hilo halitatatuliwa mapema kuna uwezekano mkubwa wa kupata matatizo makubwa zaidi katika chuo hicho kikubwa nchini.
Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Idris Kikula alisema ni kweli kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitumia matatizo ya wanafunzi katika kufanikisha mambo yao, ikiwa ni pamoja na wanafunzi ambao wanatarajia kufanya uchaguzi wao hivi karibuni.
Kikula alisema kuwa tatizo jingine linalosababisha vurugu kubwa ni pamoja na Bodi ya Mikopo kushindwa kuwapa wanafunzi fedha kwa wakati muafaka, jambo alilosema kuwa linasababishwa na wanafunzi kujaza fomu kwa makosa.
Alitoa mfano kuwa kati ya majina 400 yaliyokuwa yamebandikwa kwenye ubao wa chuo hicho, ni wanafunzi 15 tu ndio waliofanikiwa kupata fedha hizo kutokana na fomu walizojaza kutokuwa na makosa. Alisema jambo hilo lilisababisha uongozi wa chuo kuwakopesha wanafunzi zaidi ya 600 Sh100,000 kila mmoja ili kupunguza makali ya maisha na baadaye kuunda timu iliyofuatilia suala hilo Bodi ya Mikopo na kuahidiwa kuwa suala hilo lingeshughulikiwa haraka sana.
Kikula alisema kuwa wanafanya utaratibu wa kujua vinara wa mgomo huo na kwamba watakaobainika ni lazima watatimuliwa chuoni hapo kwani watakuwa wameshindwa kukidhi moja ya masharti ya chuo hicho.
Lakini Mwananchi ilitaarifiwa baadaye kuwa tayari vinara hao wameshajulikana na jana barua zao za kutimuliwa zilikuwa zikiandaliwa tayari kukabidhiwa kwa wahusika.
Polisi walifika jana asubuhi na mapema wakiwa na magari matano yaliyojaa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wakiwemo maafisa wa jeshi hilo kutoka mkoani hapa ambao hadi majira ya saa 8:00 mchana walikuwa bado wapo kwenye uwanja vya chuo hicho kuangalia usalama zaidi.
Dk. Bilali alitumia hekima kuwashawishi wanafunzi kurudi madarasani wakiwa tayari wamesababisha hasara kubwa baada ya milango tisa ya mabweni na jengo la utawala kuvunjwa. Thamani halisi ya hasara hiyo bado haijajulikana.
Bilal, ambaye ni mwenyekiti wa baraza la chuo hicho na pia ni mwalimu wa somo la fizikia, aliwaita wanafunzi wote kwenye ukumbi wa mikutano na kuzungumza nao. Baadaye wanafunzi walionekana kumuelewa na kusitisha mgomo huo.
Naye msemaji wa Bodi ya Mikopo, Cosmas Mwaisobwa alisema tayari baadhi ya wanafunzi wameshalipwa, isipokuwa wachache ambao hawana sifa kutokana na kutojaza fomu za kuomba mkopo.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar