Israel leo imeendeleza mashambulio ya kijeshi dhidi ya kundi la Hamas, katika Ukanda wa Gaza kwa siku ya saba mfululizo, ikilenga ngome 20 za kundi hilo.
Maeneo yaliyoshambuliwa na jeshi la Israel katika mashambulio ya anga ni pamoja na eneo la karakana linalodaiwa kutengeneza roketi, jengo ambalo roketi zimehifadhiwa na nyumba za baadhi ya makamanda wa kundi la Hamas, hivyo kufanya idadi ya maeneo yaliyoshambuliwa hadi sasa kufikia zaidi ya 700.
Aidha, kundi la Hamas na makundi mengine katika Ukanda wa Gaza jana yalifanya mashambulio ya roketi kwenye eneo la kusini mwa Israel. Katika mashambulio ya anga yaliyofanywa jana na jeshi la Israel, yameripotiwa kumuua kamanda mwandamizi wa kundi la Hamas.
Ndege mbili za kivita zilirusha makombora katika nyumba ya Nizar Rayan katika kambi ya Jabaliya, na kumuua kamanda huyo ambaye ni mpinzani mkubwa wa Israel, pamoja na wake zake wanne, watoto wake 10 na majirani zake wawili.
Israel inasema operesheni hiyo ya kijeshi inakusudia kuanzisha mazingira mapya ya usalama katika eneo la Wapalestina linalotawaliwa na Hamas.
Aidha, Waziri wa mambo ya nje wa Israel, Tzipi Livni jana alifanya ziara nchini Ufaransa, ambapo alikuwa na mazungumzo na Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy baada ya juhudi za kufikia amani kukwama katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo alisisitiza kuwa hawawezi tena kuendelea kulivumilia kundi la Hamas. Bibi Livni alikataa kwa mara nyingine tena wito wa Ufaransa wa kusimamisha mashambulio katika Ukanda wa Gaza ndani ya saa 48 na kusema wanachotaka wao ni kuwepo kwa suluhisho la kudumu.
Kwa upande wake Umoja wa nchi za kiarabu uliwasilisha rasimu ya azimio kwa baraza la usalama lenye kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano hayo.
Kutokana na mashambulio hayo watu katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo Israel yenyewe na baadhi ya mataifa ya Afrika, wamekuwa wakiandamana kupinga mashambulio ya Israel dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Katika hatua nyingine, Wizara ya mambo ya nje ya Israel, imesema nchi hiyo imewapatia kibali Wapalestina 367 ambao wana pasi za kigeni za kusafiria kuondoka katika Ukanda wa Gaza hii leo. Afisa wa juu wa wizara hiyo, Yigal Palmor, amesema kati ya Wapalestina hao, 168 wana pasi za kusafiria za Urusi, 85 Ukraine, 28 Moldova, 25 Kazakhstan, 15 Belarus, 33 wakiwa na pasi za kusafiria za Marekani, 7 Uturuki na 6 za Norway.
Kwa mujibu wa afisa huyo wa wizara ya mambo ya nje wa Israel, maafisa wa kibalozi kutoka nchi mbalimbali duniani na wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa ya misaada wamefanikiwa kutoka na kuingia Gaza bila ya kuwa na mipango ya awali na kuvuka maeneo ya mipaka iliyokuwa imefunguliwa kwa ajili ya kuruhusu kupelekwa kwa misaada ya kibinaadamu.
Idadi ya watu waliokufa kutokana na mashambulio hayo ya Israel yaliyoanza Jumamosi iliyopita imefikia zaidi ya 400, huku watu wengine zaidi ya 2,100 wakiwa wamejeruhiwa, 250 kati yao wakiwa katika hali mbaya.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar