Makao Makuu ya Kanisa Katoliki Vatican nchini Italia yamemnyang’anya Jimbo, Askofu wa Same, Jacob Koda, baada ya kubainika kukiuka mafundisho ya imani ya kanisa hilo. Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Joseph Chennoth alithibitisha Dar es Salaam jana kuwa Askofu Koda ametakiwa na kanisa kuacha utume huo mara moja na kupumzika ama kufanya shughuli binafsi za mafunzo.
Hata hivyo, Balozi huyo wa Papa hakufafanua zaidi kiini cha kuondolewa kwa Askofu Koda na ni mafundisho gani ya kanisa aliyokiuka, ingawa taarifa kutoka Same zilizolifikia gazeti hili jana zilidai kuwa amejiingiza katika mafundisho yaliyo kinyume cha imani ya Kikristo na ya Kanisa Katoliki.
Sambamba na kuondolewa Askofu Koda katika jimbo hilo lililoko mkoani Kilimanjaro, pia taarifa ya Askofu Mkuu Chennoth kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI amemteua Padri Rogath Kimaryo kuwa Msimamizi wa Kitume wa jimbo hilo hadi hapo litakapopata askofu mwingine.
Padri Kimaryo kabla ya uteuzi huo alikuwa Paroko wa Parokia ya Kipawa, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. “Tumemshauri kuondoka jimboni na Padri Kimaryo ataongoza jimbo hilo kwa muda mpaka hapo Baba Mtakatifu atakapomteua askofu mpya,” alisema Askofu Mkuu Chennoth.
Aidha, taarifa hiyo ya Ubalozi wa Vatican hapa nchini kwa vyombo vya habari iliyotolewa kwa gazeti hili na Katibu Mtendaji wa Habari wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Revocatus Makonge, ilithibitisha uteuzi wa Padri Kimaryo katika jimbo hilo la Same.
“Mwakilishi wa Baba Mtakatifu hapa nchini anayo heshima kutangaza kuwa Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI amemteua Padri Rogath Kimaryo (CSSP) ambaye ni Paroko wa Kipawa, Dar es Salaam kuwa Msimamizi wa Kitume mwenye mamlaka kamili na chini ya utii kwa kiti kitakatifu wa Jimbo Katoliki la Same,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa Mei 30, mwaka huu. Hata hivyo, Padri Makonge alisema TEC haina taarifa zozote za kina kuhusu suala hilo na kueleza kuwa wanachofahamu ni uteuzi wa Padri Kimaryo kupitia taarifa hiyo ya Mwakilishi wa Papa nchini.
Taarifa zaidi kutoka katika ofisi za Ubalozi wa Vatican Dar es Salaam zilieleza kuwa Padri Kimaryo atakabidhiwa jimbo hilo kwa usimamizi rasmi kesho katika Ibada ya Misa itakayoongozwa na Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo katika Kanisa Kuu la Same na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa kanisa hilo akiwamo Askofu Mkuu Chennoth.
Bila kufafanua zaidi, Askofu Mkuu Chennoth alisema Kanisa Katoliki huwa lina utaratibu wa kumteua Msimamizi wa Jimbo linapotokea hitaji kama hilo hivyo ni kitu cha kawaida ndani ya kanisa pindi panapoonekana umuhimu wa kufanya hivyo.
Askofu Koda aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II kuwa Askofu Mpya wa Same Septemba 1999 kuchukua nafasi ya Askofu Josephat Lebulu aliyehamishiwa katika Jimbo Kuu la Arusha.
Padri Kimaryo ambaye ni Padri wa Shirika la Roho Mtakatifu alitunukiwa Udaktari wa Sheria nchini Roma katika Chuo Kikuu cha Pontifical Gregorian na pia amefanya kazi ya kitume kama mshauri kwa miaka sita katika nyumba yao ya shirika nchini humo.
Kwa utaratibu wa Kanisa Katoliki, Papa humteua Msimamizi wa Jimbo ambaye kikanisa ni kama Mtawala ambaye hufanya kazi hiyo, mara kadhaa hutumikia katika eneo ambalo halijapewa hadhi ya Jimbo au katika Jimbo lisilo na Askofu au tatizo kama lililotokea. Katika sheria za kanisa (Canon Law), utawala wa aina hiyo unampa mamlaka mtawala kufanya kazi zote za kiaskofu isipokuwa kuuza mali yoyote ya jimbo na kutoa daraja la upadrisho.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar