Mafuta na Gesi yapo Tanga, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Bigwa, Mafia, Mandawa, Kisangire, Nyuni, Kilwa, Ruvu na Mnazi Bay tu.
SERIKALI jana ilitangaza maeneo 13 ambayo kuna uwezekano mkubwa wa kupatikana mafuta na gesi, ikimaanisha hakuna uwezekano kwa nishati hizo kupatikana visiwani Zanzibar.
Suala la mafuta na gesi limekuwa gumzo kubwa visiwani Zanzibar kiasi cha kutaka liondolewe kwenye masuala ya Muungano, licha ya mtaalamu aliyekodishwa na serikali kushauri kuhusu mafuta kueleza bayana kuwa uwezekano wa nishati hiyo kupatikana Zanzibar ni mdogo.
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alitaja maeneo ambayo yana uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa mafuta na gesi kuwa ni Tanga, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Bigwa, Mafia, Mandawa, Kisangire, Nyuni, Kilwa, Ruvu na Mnazi Bay.
Akifungua mkutano kuhusu utawala bora katika sekta ya petroli jana, Waziri Ngeleja alisema hadi sasa harakati za utafutaji mafuta nchini bado hazijazaa matunda, lakini matarajio yaliyopo ni makubwa.
Alisema utafiti wa kuwepo mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali ya nchi unafanywa na makampuni kutoka Ufaransa, Uingereza, Australia, Brazil, Canada, Norway na Dubai.
Tangu zianze harakati za utafutaji mafuta mwaka 1950 hadi sasa bado hatujapata mafuta lakini matarajio ni makubwa sana kwa sababu tuna imani na makampuni yanayofanya utafiti,†alisema Ngeleja.
Suala la mafuta limekuwa likiibuka kila mara Baraza la Wawakilishi linapokuwa na mikutano yake na mara kadhaa suala hilo huwaunganisha wawakilishi wa CCM na wa chama kikuu cha upinzani visiwani humo, CUF.
Baada ya mshauri mtaalamu kueleza kuwa uwezekano wa kupata mafuta visiwani humo ni mdogo, wawakilishi walidiriki kusema “hata hayo mafuta yakiwa madogo kiasi cha kujaa glasi, watuache tutagawana ili tujipakeâ€.
Hata hivyo, Rais Jakaya Kikwete akijaribu kutuliza moto huo wa wawakilishi, alisema hakuna haja ya kugombea kitu ambacho hakuna uwezekano wa kukipata na akaeleza kuwa tafiti nyingi zilizofanywa zimeonyesha kuwa ukanda wa eneo la Mashariki mwa Afrika hauna mafuta.
Waziri Ngeleja pia alisema sekta ya petroli inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo kupanda na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia hasa wakati huu ambao dunia imekumbwa na mtikisiko wa uchumi.
Waziri huyo alisema tayari wameliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) lianze kuagiza mafuta kupitia kampuni ya COPEC ili iwarahisishie kupata taarifa za kweli na ambazo hazitakuwa na upotoshaji.
Kuhusu suala la mikataba na rushwa, Ngeleja alisema wamejipanga vizuri kisera na kisheria na kwamba, hata mikataba iliyopo ina uwazi wa kutosha na kuna utaratibu mzuri ambao hautoi fursa ya kuingia kwenye rushwa.
Akitoa mada katika mkutano huo, Dk Inge Amundsen kutoka taasisi ya Michelsen ya nchini Norway alisema serikali inatakiwa kuwa makini katika suala la rushwa na uwazi wakati inaposaini mikataba mbalimbali, kuepuka migogoro ya ardhi na utunzaji wa mazingira.
Mmoja wa wabunge walioshiriki mkutano huo, Hamad Rashid alisema mkutano huo utawasaidia katika harakati za utafutaji mafuta na gesi na namna ya kuingia mikataba mbalimbali.
Naye Charles Keenja alisema mafunzo hayo waliyaomba kutoka kwa waziri wa nishati wa Norway wakati walipokwenda nchini humo kikazi na kwamba yatawasaidia kuwa na ufahamu mpana hasa wakati huu wanapojiandaa kutunga sheria ya mafuta na gesi mwakani.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar