CUF hatimaye wamtambua Rais Karume Zanzibar |
Tangazo hilo lilitolewa na katibu mkuu wa chama hicho Seif Sharif Hamad mkutanoni ambapo wapenzi na wanachama wa chama hicho walipinga.
Tamko la katibu mkuu Hamad limefuatia matukio mawili makubwa wiki hii. Kwanza ni la kufanya mazungumzo na rais Karume ikulu na pili mkutano wa kamati kuu ya chama hicho uliofanyika siku ya Jumamosi.
Hamad alisema kamati kuu ya CUF imeamua kuondosha msimamo wa kutomtambua rais Karume kwa vile kwa kiasi kikubwa nchi imekwama na hakuna kinachofanyika kwa maslahi na maendeleo ya Zanzibar.
Alisema uamuzi huo ulikuwa ni mgumu kufanywa kwa vile chama hicho kimekuwa kikiibiwa uchaguzi kila muongo unapofika pamoja na msimu wa uchaguzi kusababisha hasara ya maisha na mali.
CUF kwa miaka kadhaa sasa tangu mwaka 1995, 2000, na 2005 imekuwa ikigoma kuitambua serikali na baadhi ya nyakati wajumbe wake wa baraza la wawakilishi waligoma kuingia vikaoni.
Hamad alieleza kuwa kwa vile kumekuwa na njia mbali mbali ambazo CUF imekuwa ikishirikiana na serikali, imeonekana ni vyema kukiondosha kizingiti hicho cha kutomtambua rais.
Itakumbukwa mazungumzo ya kutafuta muwafaka yalikwama Februari mwaka huu kwa madai ya kutotambuliwa rais Karume na pia rais Karume amegoma kuchagua wajumbe wawili wa CUF kuingia katika baraza la wawakilishi kwa sababu hiyo hiyo.
Maelfu ya wanachama na wapenzi wa CUF waliofika katika mkutano huo walipiga mayowe na kumzomea Maalim Seif ambaye kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya siasa ilibidi ashuke jukwaani.
Wadadisi wa kisiasa wanadhani cuf itapita katika kipindi kigumu ikiwa ni mwaka mmoja tu kabla ya uchaguzi mkuu, lakini wako pia wanaodhani uamuzi huo unaweza kukifanya chama hicho kuwa imara zaidi, kwa uamuzi wake wa kusamehe dhulma wanazodai wanafanyiwa
Tidak ada komentar:
Posting Komentar