Chadema hali tete wenye viti mikoa 11 wapinga uamuzi wa Dk Slaa | |||||||
UAMUZI wa katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa wa kuwatimua maafisa wawili wa sekretarieti, umekifanya chama hicho kugubikwa na wingu zito baada ya wenyeviti wa mikoa 11 kumpinga, akiwemo katibu wa Kigoma, Msafiri Wamarwa ambaye amejitokeza kutangaza kuwatambua waliotimuliwa. Wiki iliyopita, Dk Slaa, ambaye kwa cheo chake ni mkuu wa sekretarieti ya chama hicho, alitangaza kumtimua David Kafulila kwenye nafasi ya afisa habari, sambamba na Danda Juju ambaye alikuwa akihusika na mambo ya Bunge kwa madai kuwa wawili hao waliofananishwa na sisimizi walionyesha utovu wa nidhamu na kuvujisha siri za chama. Jana, wenyeviti wa mikoa hiyo 11, ambayo baadhi iko nyanda za juu kusini, mashariki na kaskazini (majina yao tunayo), waliweka bayana kwamba uamuzi wa Dk Slaa haukubaliki hadi atakapotoa sababu za msingi za kuwafukuza maafisa hao. Viongozi hao wakiweka sharti la kuhifadhiwa majina ili wajipange vema kwa ajili ya mkutano wa Kamati Kuu uliopangwa kufanyika Novemba 27 na 28, walisema uamuzi huo unaonekana kulenga watu ambao walikuwa upande wa naibu katibu mkuu, Zitto Kabwe na kutaka usitishwe mara moja. "Hatuwezi kuendesha chama kwa visasi... mambo ya uchaguzi wa Septemba yalishapita, sasa tunavyoanza kuleta chuki za kipuuzi tunataka chama kife," alihoji mwenyekiti wa moja ya mikoa ya kaskazini. Mwenyekiti mwingine kutoka moja ya mikoa wa kusini aliweka bayana kwamba Chadema ni chama ambacho kipo kwa ajili ya makundi ya watu wote si tabaka fulani. "Angalia Dk Slaa anamwita Kafulila sisimizi, hii ni dharau ya hali ya juu. Ina maana kuna sisiminzi na tembo ndani ya chama... hivi kweli tutafika kwenye uchaguzi kama watu wanakuwa na roho mbaya na dharau za kiasi hiki," alihoji mwenyekiti huyo kutoka kusini. Mmoja wa wenyeviti kutoka moja ya mkoa wa mashariki aliweka bayana kwamba chama hicho kwa sasa kinaelekea kugawanyika rasmi kama kutakuwa na mwendelezo wa majeraha ya uchaguzi wa Septemba. Aliongeza kwamba mambo yaliyotokea wakati wa uchaguzi yaliisha hivyo kambi za mwenyekiti Freeman Mbowe na Zitto hazitakiwi kuendelea, bali kujenga chama kiwe kimoja kinachotakiwa kushinda uchaguzi mwakani. Wenyeviti hao wengine waliisisitiza kwamba kimsingi wanapinga vikali uamuzi huo wa Dk Slaa, lakini hawataki kuanza kunukuliwa majina kwenye vyombo vya habari kwani wanamsubiri Dk Slaa kwenye Kamati Kuu aeleze sababu za msingi na kutosha. Wakati wenyeviti hao wakiweka msimamo wao kwa nyakati tofauti, Wamarwa ambaye anatoka mkoani Kigoma ambako Kafulila ameonyesha nia ya kutaka kuwania ubunge wa jimbo la Kigoma Kusini, aliweka bayana kwamba hatambui uamuzi wa kuwavua madaraka wawili hao. Kwa mujibu wa Marwa, mkoa haujapewa taarifa na makao makuu juu ya uamuzi huo na hivyo bado wanawatambua kama watendaji wa Chadema. “Habari hizi tumeziona kwenye vyombo vya habari, lakini mimi kama katibu wa mkoa, ofisi yangu haijapewa taarifa zozote za kimaandishi zinazoeleza juu ya kufutwa nyadhifa kwa Kafulia na Danda, hivyo sisi bado tunawatambua,†alisema Wamarwa. Mwananchi imedokezwa kuwa hadi jana jioni, Kafulila hakuwa amepewa barua rasmi ya kumvua wadhifa wake. “Hata kama tutapewa taarifa na makao makuu, tutakaa kama uongozi wa Chadema mkoa na kujadili maamuzi hayo na tutatoa maamuzi yetu,†alisisitiza Wamarwa. Alifafanua kwamba hivi sasa chama kimejaa mamluki ambao kazi yao ni kuhahakikisha wanawagombanisha baadhi ya viongozi wa juu ili kuhakikisha Chadema haifanyika vizuri uchaguzi wa 2010. “Haya mambo yakiendelea chama kitakufa kama ilivyokuwa kwa vyama vingine vya upinzani. Umefikia wakati wa kuwatimua wale wote wanaoendeleza mambo yaliyozimwa katika uchaguzi mkuu wa chama Septemba mwaka huu,†alisema Wamarwa. Wamarwa pia alisema kuna haja ya kuitishwa haraka kikao cha Baraza Kuu la Taifa ili kujadili mwelekeo wa chama hicho. "Siwezi kusema tutaamua nini kwa sababu ni lazima tukae uongozi mzima wa mkoa... lakini pamoja na hayo Baraza Kuu la Taifa inabidi likutane mara moja kwa sababu hali inaonekana inakwenda vibaya kila siku zinavyozidi kwenda," alisema Wamarwa. "Hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa, Chadema tumeshinda Kigoma kwa asilimia 70, na Kigoma Kusini ambako Kafulila atagombea ubunge tumeshinda kwa asilimia 80, hivyo ipo haja ya kulizungumza hili kwa umakini mkubwa." Tayari Zitto ameshaeleza bayana athari za maamuzi hayo hasa katika kipindi ambacho Chadema imetoka katika mtikisiko uliosababishwa na uchaguzi wa viongozi wake. Zitto, ambaye yuko nje ya nchi, alisema chama kilitakiwa kuwa makini katika kufikia uamuzi huo, hasa kwa kuzingatia kuwa Kafulila atagombea ubunge wa Kigoma Kusini na mustakabali wa chama kwa sasa. Lakini, Dk Slaa aliliambia gazeti hili kuwa uamuzi huo ni kwa maslahi ya chama na haulengi kundi fulani na kutamba kwamba kutimuliwa kwa wawili hao hakutasababisha mpasuko. Alisema ni bora chama kupasuka kuliko kufa. Wakati chama kikijiweka sawa baada ya kuwatimua wawili hao, Kafulila atakuwa mmoja wa wachangiaji kwenye mkutano wa taasisi ya Mo Ibrahim, kwa mujibu wa barua ya mwaliko. Taasisi ya Mo Ibrahim imekuwa ikijihusisha na utekelezwaji wa dhana ya utawala bora barani Afrika na imekuwa ikitoa tuzo kwa rais mstaafu kwa kuangalia jinsi alivyotekeleza dhana hiyo wakati akiwa madarakani. "Hii si heshima kwangu tu, bali kwa taifa na chama changu cha Chadema," alisema Kafulila akizungumzia mwaliko huo. "Nitatumia nafasi hii kutowaangusha Watanzania kwa ujumla katika kujadili mambo ya msingi yanayohusu bara la Afrika." Kafulila ni mmoja wa vijana wa Chadema ambao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika chama. Aliwahi kuanguka ghorofani akiwa katika harakati za kujenga chama. |
Sabtu, 14 November 2009
Langganan:
Posting Komentar (Atom)
Tidak ada komentar:
Posting Komentar