DAWA ya mpasuko wa wabunge ndani ya CCM inaonekana kuwa ngumu, kutokana na
kamati ya wazee wa CCM kushuhudia uhasama wa wazi, huku wakiendelea ‘kupashana’
kwa lugha kali.
Kamati hiyo inayoongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi imemaliza kazi yake, lakini wadadisi wa mambo ndani ya chama hicho wamekiri kuwa chuki na uhasama huenda visimalizike.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilisema Katibu wa Itikadi na Uenezi, John
Chiligati, alisema chanzo cha mpasuko ni wanamtandao ambao wamepasuka katikati hivyo
kuwepo kundi la Edward Lowassa na Samuel Sitta.
Inadaiwa alisema watu hao ndio wamesababisha mpasuko mkubwa hivyo akashauri kamati hiyo ya wazee wa CCM, iwaite Lowassa, Sitta na watu wao wa karibu, Rostam Aziz na Katibu Mkuu, Yussuf Makamba.
Mpasha habari huyo alidai kuwa iwapo kamati hiyo itakaa nao ili kupata ufumbuzi wa kudumu, pia mmoja wa wajumbe, Abdulrahaman Kinana, asaidie kwa karibu. Ilielezwa kuwa Chiligati anaamini kuwa Kinana anaweza kusaidia kuondoa mpasuko huko kutokana na kuyajua makundi hayo vizuri.
Lakini wapasha habari hao walidai kuwa mbunge wa Nzega, Lucas Selelii alisema chanzo cha mpasuko huo ni Bunge kukubali kuunda kwa tume ya kuchunguza kampuni ya kufua umeme ya Richmond.
Alisema wabunge tangu wakati huo waligawanyika wakiwamo waliounga mkono kuundwa kwa
kamati na wengine wakawa wanapinga na akatoa mfano wa hoja ya mbunge wa Ukonga, Dk Makongoro Mahanga.
Mbunge huyo pia alisema kutokana na mgawanyiko huo ndiyo maana kamati ilipata wakati mgumu wa kutimiza majukumu yake ikiwamo kunyimwa baadhi ya nyaraka na watendaji wa Serikali kwa kile anachoamini kuwa yalikuwa maagizo kutoka kundi la Lowassa.
Inadaiwa alimtetea Spika Sitta kuwa hakuwa na hila kuunda kamati hiyo na akaeleza kuwa hata baada ya kamati kukamilisha kazi yake ilipeleka kwa Rais ripoti hiyo kabla ya mwezi mmoja kuwasilishwa bungeni.
Alisema hata vyombo vya ulinzi na usalama vilikuwa vinajua kinachofanyika na kamati hiyo, hivyo akasema hakukuwa na mipango ya kuwaonea baadhi ya watu kama ambavyo baadhi ya wabunge
wanataka jamii iamini.
Mbunge wa Kishapu, Freddy Mpendazoe, inadaiwa kwamba alishangaa kuwapo viongozi ndani ya CCM ambao wanapinga wabunge wanaopigia kelele ufisadi na akasema kama kufanya hivyo kwa mbunge wa CCM ni dhambi, basi chama hicho kibadilishe Katiba inayotamka kuwa rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala sitapokea rushwa.
Mbunge huyo pia alishangaa viongozi wa CCM ambao wanamshambulia Mwenyekiti Mtendaji wa IPP
Reginald Mengi kuwa si wanachama wa CCM wakati wanakwenda kumwomba fedha za
uchaguzi.
Wakati Mpendazoe anatoa shutuma hizo, Makamba alisimama na kutaka thibitisho wa madai hayo ndipo mbunge huyo inadaiwa akasema anazo taarifa zote.
Lakini Mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombale-Mwiru aliomba mwongozo wa Mwenyekiti
na kuhoji sababu ya mbunge huyo kumtukuza Mengi kwenye kikao hicho, wakati si mbunge
ndipo Mpendazoe akajibu kuwa anafanya hivyo kwa vile kuna viongozi wa chama hicho
walipinga wabunge wanaochangiwa fedha za Vicoba na Mwenyekiti huyo wa IPP.
Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba alisema chanzo cha mpasuko wa wabunge ni madaraka na lengo ni kuwaondoa baadhi ya watu kama Lowassa kwenye ulingo wa siasa.
Naye Rostam Azizi alisema ni jambo la aibu wabunge wa CCM kuitwa mbele ya kamati ya
wazee wa CCM na jambo hilo akasema halifai kujivunia kwani linaonesha namna chama
hicho kilivyogawanyika.
Alisema tuhuma juu ya kampuni ya Kagoda inayodaiwa kuwa ni yake hazina ukweli wowote na wanaofanya hivyo wanamsulubu bure kwani si ajenda ya CCM bali ni ya Chadema, akashangaa iweje wabunge wa CCM washikie bango jambo ambalo si ajenda yao. Alisema kwamba yeye anaamini kuwa kumsulubu yeye au Lowassa juu ya suala la Richmond ni kukikusulubu chama.
Rostam pia anadai kusema kwamba mpasuko kati ya wabunge na wabunge wa chama hicho ni
uchaguzi wa mwaka 2005 baada ya watu kushindwa kupata urais ndipo wakaanzisha vita na
kundi la watu ambao waliingia madarakani.
Mpasha habari alisema Rostam alisema kwa masikio yake aliwahi kuwasikia baadhi ya wabunge wakiapa kuwa wataiaibisha Serikali ya sasa wakati wakinywa chai kwenye mgahawa wa Bunge.
Kada huyo wa CCM anadai pia kueleza kuwa kutokana na hali hiyo Sitta akawa adui
mkubwa wa Lowassa na yeye mara kadhaa alijaribu kuwapatanisha, lakini ilishindikana
hivyo Sitta na wabunge wake wakawa na kasi ya kumfanyia hujuma Lowassa likiwamo
suala la Richmond.
Kuhusu ripoti ya Richmond, Rostam alisema tangu mwanzo kulikuwa na hila mbaya ndio
maana yeye alinyimwa fursa ya kutoa maoni yake mbele ya kamati hiyo.
Lakini Rostam pia alienda mbali na kutaka chama kuanzia sasa kiwachukulie hatua kali wabunge wanaoikosoa Serikali. Kuhusu kuumizwa kwake kisiasa alisema licha ya kuwa ameumizwa sana kuhusu jambo hilo yeye tayari ameshasamehe, kwani Mungu amemjaalia moyo wa kusamehe.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar