Malecela ashauri Waziri Sophia Simba apimwe akili Mirembe | |||||||
WAZIRI mkuu wa zamani, John Malecela jana alimshukia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba akisema kuwa tuhuma alizozitoa dhidi yake zinatokana na waziri huyo kuwa mgonjwa wa akili, huku mkewe ana Kilango, akimshangaa kwa kukalia tuhuma hizo kwa kipindi kirefu. Mbali na wanandoa hao, mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi naye alipuuza tuhuma alizorushiwa na Waziri Simba akisema kuwa hawezi kubishana na mjinga. Malecela, Kilango na Mengi ni miongoni mwa watu kadhaa walioshambuliwa na Waziri Simba Jumatano, akiwatuhumu wanandoa hao kuwa walichukua fedha za kifisadi wakati walipofanya harusi yao mjini Dodoma na katika kampeni za urais za mwaka 2005, huku akimtuhumu Mengi kuwa anatumia vyombo vyake vya habari kuichafua CCM na serikali yake kwa maslahi binafsi. Wote watatu hawakuingia ndani kukanusha madai hayo ya Simba wala kutoa ufafanuzi, na badala yake Mengi na Malecela walimrushia maneno makali wakimwita kuwa ni mgonjwa wa akili, asiye na maadili, mropokaji na ambaye si msafi huku Kilango akisema kuwa bado anatafakari. Malecela, ambaye alikuwa waziri mkuu na makamu wa kwanza wa rais (1990 hadi 1994), alidai kuwa Simba ni mgonjwa wa kichwa na akili hivyo anapaswa kupelekwa Hospitali ya Mirembe kabla ya kurudi Dar es Salaam baada ya bunge kuisha. Hospitali ya Mirembe iliyo mjini Dodoma hujishughulisha zaidi na tiba ya watu wenye matatizo ya akili. Kama ilivyokuwa kwa Kilango ambaye alidai juzi kuwa mashambulizi dhidi yake yanatokana na mumewe, Malecela naye jana alidai kushambuliwa kwake ni kutokana na mkewe Kilango kwamba ameona azungumze kwa kifupi kuhusu hali halisi ya akili ya Simba. "Najua chanzo kikubwa ni mama (Kilango), yeye leo ametoa taarifa yake, lakini na mimi ninalo moja dogo la kusema kijana ambalo ni ushauri kwa Waziri Simba," alisema Malecela. "Simba ni mgonjwa, ana matatizo ya akili kichwani, namshauri apelekwe au aende Mirembe akapimwe akili na kupata matibabu kabla hajarudi Dares Salaam." Mzee Malecela ambaye ni mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu na makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, alisema Simba atafanya kosa kama atarudi Dar es Salaam bila kwenda Mirembe kupima akili na kupata matibabu. "Asirudi Dar es Salaam bila kupita Mirembe kupima akili, kwa maana atakuwa amepoteza fursa ya kujua matatizo aliyonayo kichwani kwake," alisisitiza. Kwa sasa Waziri Simba yuko Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge na alitoa kauli za kumshambulia Malecela, Kilango, Mengi na Mwakyembe kwenye mikutano inayoendelea baina ya wabunge wa CCM na Kamati ya Mwinyi ya kutafuta chanzo cha kutoelewana ndani ya chama hicho. Malecela, ambaye aliwahi kuteuliwa kuwa mmoja wa watu sita wenye busara katika nchi za Umoja wa Madola mwaka 1985, hakueleza kama ana ushahidi wa madai yake. Hata hivyo, Simba aliwahi kuugua akiwa Afrika Kusini na baadaye Hindul Mandal akiwa anasumbuliwa na kizunguzungu na kutapika, ugonjwa ambao waziri huyo aliwakariri madaktari wakisema utapona taratibu. Hata hivyo, alipoulizwa iwapo tuhuma za yeye kufadhiliwa na Patel katika harusi yake na kupewa kiasi hicho cha fedha Sh200 milioni za kampeni za Urais mwaka 2005, Malecela alisema tuhuma hizo zimetolewa na mgonjwa. Naye mbunge wa Same Mashariki, Kilango alionyesha kushangazwa na tuhuma hizo na kumshangaa waziri huyo kukalia tuhuma nzito alizozitoa kwa muda mrefu bila kuzifikisha kwenye vyombo vya sheria. Kilango na Malecela walituhumiwa na Simba Jumatano kuwa nao walichukua fedha za ufisadi, akidai kuwa harusi yao ilifadhiliwa na Jeetu Patel, ambaye ni mtuhumiwa wa ufisadi na hali kadhalika kampeni za urais za Malecela za mwaka 2005. Katika tuhuma zake, Waziri Simba alidai kuwa Kilango ni mnafiki na si msafi kiasi cha kuwanyooshea wenzake vidole na kwamba kelele zake zote zimetokana na kukosa kuwa mke wa rais baada ya Malecela kuenguliwa mapema na CCM kwenye mchakato wa kumpaya mgombea wake. Lakini jana, Kilango alisema hatakatishwa tamaa na tuhuma hizo nzito, ambazo alisema bado anazitafakari, ili kubaini kiini chake na sababu za kutolewa sasa katika kipindi ambacho vita dhidi ya ufisadi imepamba moto. Kilango, ambaye mwaka huu alitunukiwa Tuzo ya Mwanamke Jasiri na serikali ya Marekani, alimshangaa Simba kukaa kimya na tuhuma hizo tangu 2005 wakati vyombo vya dola vipo. "Kama Mheshimiwa Simba alikuwa na ushahidi wa tuhuma nzito kama hizo tangu mwaka 2005 kama ambavyo anataka Watanzania waamini, bado haiingii akilini ni kitu gani kilichomfanya asitoe taarifa hizo katika vyombo vya dola,? alihoji Kilango. Kilango alifafanua kwamba Simba ni waziri mwenye dhamana ya utawala bora ambaye ana vyombo vya uchunguzi chini yake kama Takukuru, lakini akashangaa kutovitumia. ?Ni imani yangu kwamba, mheshimiwa Simba ambaye ni waziri katika Ofisi ya Rais atapimwa na wananchi kama malumbano anayoyaanzisha sasa yana chembe ya ukweli kiasi gani au ni kujaribu kuwahamisha Watanzania katika vita nzito dhidi ya ufisadi,? alisema. Katika taarifa yake ya maandishi, Kilango alisema asingependa kuingia katika malumbano na waziri huyo kwa kuwa itawapa taabu Watanzania kutofautisha pumba na mchele. Kauli ya Simba inaonekana kuibua mjadala mpya katika vita dhidi ya ufisadi katika kipindi hiki ambacho kimetawaliwa na malumbano makali baina ya wabunge wanaojinadi kuwa ni makamanda wa vita ya ufisadi na wale wanaodai kuchukulia vita hiyo kuwa ni ya kukichafua chama na serikali. Malumbano hayo yamefikia kipindi ambacho wabunge wenyewe wameanza kuhoji maamuzi yao ya kukubaliana na ripoti ya kamati teule iliyochunguza kashfa ya mchakato wa utoaji wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura kwa kampuni ya Richmond Development na kutaka uchunguzi mpya ufanyike ukihusisha tume huru. Tayari mawaziri wawili, Dk Makongoro Mahanga na Simba wamejitokeza kumtetea Edward Lowassa ambaye aliachia wadhifa wake wa waziri mkuu kutokana na kutakiwa na ripoti hiyo kufanya maamuzi kwa kutumia busara yake kutokana na kashfa hiyo. Hata mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge, ambaye alijiuzulu uwaziri baada ya kutajwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada, naye amejikuta akipata watetezi, akiwemo Waziri Simba ambaye alielezea kuwa uchunguzi umeonyesha kuwa mwanasheria huyo mkuu wa zamani wa serikali hana hatia. Nje ya Bunge, Mengi ndiye aliyeguswa zaidi na Waziri Simba na jana aliongea na waandishi wa habari kuhusu tuhuma hizo akisema: "Dont argue with a fool because people may not know the difference between you and the fool (usibishane na mjinga kwa sababu watu wanaweza kushindwa kufahamu tofauti yako na huyo mjinga)." Hata hivyo, Mengi alisema wakati mwingine unalazimika kujibu hoja "unapoona mtu anapotosha mambo kwa makusudi" na akaeleza kuwa Waziri Simba si mtu msafi hivyo ni vema katika vita ya ufisadi inayoendelea akakaa kimya kuliko kujitokeza na kuropoka. Mengi, ambaye amekuwa akionekana kuunga mkono kundi linalopambana na ufisadi, alimtaka Waziri Simba kutafuta ushauri kutoka taasisi za serikali, ikiwemo Idara ya Usalama wa Taifa, kabla hajazungumza. Hata hivyo, Mengi hakutoa maelezo ya tuhuma kwamba amekuwa akitumia vyombo vyake vya habari kuendesha kampeni zinazoichafua CCM na serikali yake kwa maslahi yake binafsi na badala yake alielezea uanachama wake kwenye chama hicho tawala. "Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikituhumiwa na baadhi ya viongozi wa CCM kwamba, mimi si mwanachama wa chama hicho na kwamba sitoi misaada ya hali na mali kwa chama," alisema Mengi katika mkutano wake na waandishi. "Kwanza, kuhusu kuropoka kwamba sitoi misaada kwa CCM, hilo ni jambo linalozushwa na watu binafsi na kwa malengo binafsi. Viongozi wakuu wa CCM ambao ni waadilifu na wanaosimamia ukweli wanajua undani wa jambo hili. Siwezi kusema nasaidia nini CCM, kwa kuwa itakuwa ni kukidhalilisha chama changu. "Pili, kuhusu uanachama wangu wa CCM, napenda kuwaambia kwamba mimi ni mwanachama wa CCM tangu tarehe 18 Aprili,1977 na kadi yangu ni na. B124595, iliyotolewa na tawi la Kisutu, wilaya ya Ilala, mkoa wa Dar es Salaam." Katika mkutano huo, Mengi alitumia vielelezo kujibu tuhuma kwamba amejiunga na CCM hivi karibuni. Mengi alisema anashangaa kauli za Waziri Simba na katibu wa CCM mkoani Dares Salaam, Shaaban Kilumbe kwamba, alipita matawi yote na kubaini hakuna sehemu ambako aliwahi kuwa mwanachama. "Lakini wakati mwingine inawezekana hakuona kweli kwa sababu labda hajui kusoma... ni kitu kibaya sana kujaribu kuzungumzia mambo yanayohusu kusoma wakati hujui kusoma, labda Reginald kasoma John," alituhumu. Aliongeza kwamba wanaosema CCM hakuna kiongozi msafi ni dhahiri wao ndiyo wameingia katika chama hicho hivi karibuni na kusisitiza: "Ningetoa ushauri waondoke na watuachie chama chetu kwa kuwa hawafahamu misingi imara ya CCM." Tangu Kamati ya Mwinyi ianze kazi ya kuwahoji wabunge mjini Dodoma, kumekuwepo na kurushiana maneno ya kudhalilishana baina ya wabunge hao wa chama tawala, kwa ufisadi na kupokea fedha zinazotokana na ufisadi. |
Sabtu, 07 November 2009
Malecela ashauri Waziri Sophia Simba apimwe akili Mirembe
Langganan:
Posting Komentar (Atom)
Tidak ada komentar:
Posting Komentar