Mkutano wa Obama na Netanyahu.
Mkutano kati ya Rais Barack Obama na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, katika Ikulu ya Marekani hapo jana ulishindwa kuleta mafanikio yeyote. Ishara kuwa mambo hayakuwa sawa, ni pale Netanyahu alipoondoka Ikulu ya Marekani, saa moja baada ya mkutano na mwenyeji wake, rais Obama, bila ya kupigwa picha ya pamoja kama ilivyo kawaida.
Kwa mara ya kwanza, waandishi wa habari hawakuruhusiwa katika mkutano huo, kati ya Rais Obama na Waziri mkuu Netanyahu. Hili halikuwa kawaida, ndio ilikuwa ishara za kwanza kwamba uhusiano kati ya washirika hawa wawili ulikuwa unayumba yumba.
Baada ya saa moja ya mazungumzo, Netanyahu aliondoka, bila hata ya kupiga picha pamoja na mwenyeji wake, kama ilivyo desturi ya ziara yeyote ya kiongozi katika Ikulu ya Marekani.
Rais Obama, Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.Taarifa fupi kutoka Ikulu ya White House, ilisema Obama alimhakikishia Netanyahu kuwa Marekani itaendelea na wajibu wake wa kuhakikisha Israel iko salama, na pia walizungumzia masuala mengine ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Taarifa hiyo iliongeza kwamba Obama na Netanyahu pia walijadili suala la Iran na mkakati wa kufufua mazungumzo ya amani Mashariki ya Kati. Kabla ya mkutano huo, Netanyahu alisema yuko tayari kuanzisha majadiliano, lakini kila kukicha matumaini ya uwezekano wa mazungumzo hayo yanazidi kufifia.
Mkutano kati ya Obama na Netanyahu, ulikuwa ni kama wa ghafla, kwani ni Jumapili ndipo taarifa zilipotoka zikisema kutakuwepo na mkutano huo, baada ya Netanyahu kuwa tayari amewasili Washington. Maafisa wa pande zote mbili waliyakana madai kuwa mualiko alioupata Netanyahu wa dakika za mwisho unatoa sura kuwa utawala wa Obama unavunjika moyo na jinsi Netanyahu anavyokabiliana na suala zima la Mashariki ya Kati.
Mkutano kati Hillary Clinton na Mahmoud Abbas.Nchi za Kiarabu pia zimeanza kuonyesha kutoridhika na jinsi Marekani inavyoshindwa kuiwekea mbinyo Israel. Matamshi ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton alipokuwa mashariki ya Kati, yalitia walakin zaidi, msimamo wa Marekani, Clinton alikosolewa kwa kumlimbikizia sifa Netanyahu kuhusiana na ujenzi wa makaazi, ingawa baadaye Clinton alijirudi na kusema msimamo wa Marekani ni ule ule.
" Sera yetu kuhusiana na ujenzi wa makaazi ya kiyahudi haijabadilika, nataka niseme tena sera yetu haijabadilika, hatukubali uhalali wa shughuli ya ujenzi wa makaazi ya kiyahudi. Kile ambacho tumepokea kutoka Israel, ni kusitishwa kwa ujenzi wa makazi mapya." alisema Clinton.
Netanyahu jana alimtolea wito Rais Mahamoud Abbas ambaye anaonekana ni mwenye msimamo wa kadri, akisema wakati ni sasa wafanye kila juhudi kufufua mazungumzo ya amani. Kabla ya mkutano huo wa White House, Mamlaka ya Palestina ilionya huenda machafuko yakalikumba eneo la Mashariki ya Kati iwapo Marekani itashindwa kuishurutisha Israel isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa kiyahudi. Tangazo la Abbas kwamba hatogombea urais Januari, inatia walakini zaidi matumaini kuwa Obama atafaulu kuwashawishi Waisraeli na Wapalestina kurejea katika meza ya mazungumzo.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar