|
BAADA ya Kamati inayoongozwa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kuzungumza na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi na kuibuka malumbano, kejeli na matusi kwenye mkutano huo, imebainika kuwa sasa mpasuko si tu miongoni mwa wabunge; bali umesogea hadi kwenye Baraza la Mawaziri na kugawa mawaziri hao.
Uchunguzi wa Raia Mwema, ukihusisha mazungumzo na baadhi ya wabunge na mawaziri, umebaini kuwa mpasuko katika baraza la mawaziri kwa kiasi fulani umechukua sura tofauti na ule wa wabunge wa CCM.
Katika Baraza la Mawaziri, hali ni tofauti. Siku kadhaa mara baada ya mkutano wa Mwinyi, Dodoma, wapo mawaziri walioanza kuwapuuza manaibu mawaziri wao, lakini pia wapo manaibu mawaziri walioanza kuwapuuza mawaziri wao, hali inayotajwa kuwa huenda ikasogea hadi kwa watendaji wa chini kwenye wizara na hatimaye kugawa watendaji wote.
Lakini pia katika mazungumzo hayo ya Raia Mwema, pia imebainika kuwa kuna baadhi ya wizara zenye mawaziri wanaofanana kimtazamo wakiwa kundi moja kwenye mpasuko huo; hali inayotajwa kuwa huenda ikazua mvutano kama watendaji wengine waandamizi wizarani watakuwa na misimamo pinzani.
Mpasuko huo chanzo chake kinatajwa kuwa kashfa ya Richmond, na hususan kuhusika kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwenye sakata hilo ambapo mawaziri na manaibu mawaziri wanaodaiwa kuwa karibu naye wameendelea kumtetea kwa siri na hadharani; huku wengine wakitafsiri hatua hiyo kuwa ni upuuzi na hata kuwaona wenzao wanaoendesha harakati hizo ni wapuuzi.
Mmoja wa mawaziri hao ni Sophia Simba, ambaye sasa si tu imedaiwa anatazamwa kwa jicho tofauti na baadhi ya mawaziri wenzake, lakini pia CCM imeanza kukana baadhi ya shutuma alizotoa kwa baadhi ya watu katika juhudi zake za kutetea watuhumiwa wa kashfa mbalimbali. Simba anadaiwa kueleza kuwa Mfanyabiashara Reginald Mengi, si mwanachama wa chama hicho.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kati ya mawaziri 26 waliopo ukimwondoa Waziri Mkuu, 10 wamedaiwa kuwa na msimamo unaofanana na baadhi ya wabunge wapambanaji wa ufisadi wakiwa na msimamo watuhumiwa wa ufisadi waadhibiwe, wakati mawaziri wengine wanane wakiwa katika kundi la utetezi.
Mawaziri wanaodaiwa kuwa na msimamo wa kupinga ufisadi ukiwamo wa Richmond ni pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Uvuvi, John Magufuli, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Mary Nagu, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Bunge, Philip Marmo.
Wengine ni Waziri wa Afya, Profesa David Mwakyusa ambaye anatajwa kuwa na msimamo wa chini chini, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Celina Kombani, Waziri wa Afrika Mashariki, Diodorous Kamala na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Margaret Sitta.
Mawaziri wanaodaiwa kuwa msimamo wao haueleweki katika sakata la Richmond ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, dk. Hussein Mwinyi, Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Waziri wa Kilimo, Stephen Wasira.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kundi la mawaziri wenye msimamo mkali wanaotaka hatua kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa, wengi wao wamekuwa na rekodi nzuri kiutendaji ikilinganishwa na wale watetezi wa watuhumiwa.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na Raia Mwema wamedai kuwa mawaziri wengine wanane msimamo wao umeshindwa kubainika moja kwa moja kutokana na kuwapo katika kila kundi.
Katika mkutano uliopita wa Bunge, utekelezaji wa lala salama wa mazimio ya Bunge kuhusu Richmond ulipaswa kutolewa taarifa na serikali lakini haikuwa hivyo, bila kuelezwa sababu za wazi.
Uchunguzi huo wa muda mrefu wa Raia Mwema bungeni pia umebaini kuwa athari za makundi kwa kiasi fulani zimekuwa zikimgusa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye ndiye aliteuliwa na Rais baada ya Lowassa kujiuzulu.
Uchunguzi huo umebaini kuwa katika mkutano wa 16 wa Bunge na baadhi ya vikao vya mkutano wa 17 uliokwisha, hivi karibuni, wakati akitoa hoja au kujibu maswali ya papo kwa papo yenye utetezi wa Serikali ni sehemu ya mawaziri wachache tu wamekuwa wakimpongeza kwa kumpigia makofi na wengine wakibaki kuduwaa, wengine wakiwa katika mazungumzo yao.
Kutokana na hali hiyo, mmoja wa wabunge amedai kuwa wapo mawaziri wasiompa nafasi ya heshima na utiifu unaostahili Waziri Mkuu Pinda na kwamba, wameendelea kuwa watiifu zaidi kwa kundi lao kuliko kwa waziri mkuu.
Wizara ambazo zimejipambanua kuwa na waziri mwenye msimamo wa utetezi kwa Lowassa na watuhumiwa wengine ni Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais – Utawala Bora, inayoongozwa na Sophia Simba.
Wizara nyingine ambazo zimebainika kuwa na mawaziri wenye misimamo ya makundi ni pamoja na Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, inayoongozwa na Profesa Juma Kapuya, na Naibu wake Dk. Makongoro Mahanga.
Kapuya alitajwa na kundi mojawapo kwenye mpasuko huo kuwa ni kati ya watu wanaopaswa kuchukuliwa hatua akidaiwa kumtetea Lowassa kwa gharama za wanasiasa wengine akiwamo Spika wa Bunge, Samuel Sitta. Naibu wake, Makongoro naye pia alijipambunua kuwamo kwenye kundi la Lowassa, wakati wa mkutano wa Mwinyi.
Baadhi ya wabunge pia wanaitazama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa inaongozwa na viongozi wenye mgongano wa makundi, japokuwa ikidaiwa kuwa Naibu Waziri Khamis Kagasheki, amejitahidi kwa muda mrefu kuficha hisia zake tofauti na Waziri wake, Lawrance Masha, anayedaiwa kuwa kundi la Lowassa.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wabunge waliozungumza na Raia Mwema kutoka makundi yote wamebainisha matarajio yanayozidi kukinzana mara baada ya kukamilika kwa mkutano kati yao na Kamati ya Mwinyi.
Wakati upande mmoja ukiendelea kusisitiza kuwa watuhumiwa wenye nyadhifa katika chama hicho wang’olewe, wenzao wamekuwa na msimamo tofauti.
Hata hivyo, kundi la wabunge wanaotaka wenzao watuhumiwa watimuliwe ndilo linaonekena kuwa na nguvu zaidi hata mbele ya wananchi na taasisi nyeti zikiwamo za elimu ya juu nchini kama ambavyo imekuwa ikiandikwa na baadhi ya magazeti nchini.
Kwa upande mwingine, hali ya kuwapo kwa kile kinachoelezwa kuwa ni mvutano huenda ikaendelea. Kuwapo kwa dalili hizo kunatokana na kuendelea kukinzana kati ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta na baadhi ya wanasiasa wa kundi linalomwandama, akiwamo Kingunge Ngombale-Mwiru.
Kingunge katika mkutano uliopita wa NEC-CCM Dodoma aliripotiwa kutaka Spika Sitta ang’olewe kwa kuwa anaendesha Bunge vibaya kwa kuruhusu mijadala ya ufisadi na hivyo kuhatarisha chama na serikali na kuimarisha hoja yake kwa kusema ubaya wa Spika unathibitishwa na hatua yake ya kuandika kitabu kinachoitwa “Bunge lenye Meno” akishirikiana na wabunge wengine machachari, akiwamo Dk. Harrison Mwakyembe.
Inaelezwa kuwa Kingunge alirejea msimamo wake huo katika mkutano wa Mwinyi lakini akionyesha kukejeli msimamo huo, Spika wa Bunge wakati akizungumza bungeni muda mfupi kabla ya kuahirishwa kwa Bunge, alijigamba kuwa Bunge lake bado lina meno.
Sitta alitamka; “Ni Bunge lenye meno” wakati akielezea uamuzi wa kuwatuma wabunge kwenda eneo la Loliondo lenye mgogoro kati ya wananchi na mwekezaji, mgogoro ambao serikali kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsha Mwangunga, iliwasilisha ripoti yake iliyotokana na kamati aliyounda kubaini kama kulikuwa na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Ripoti hiyo ya Mwangunga ilikataliwa na Bunge baada ya Waziri kueleza kuwa hapakuwa na haki za binadamu huku wananchi walioathirika wakieleza kuwa haki zao zilikiukwa, ikiwa ni pamoja na kuchomewa makazi na karaha nyingine zikiwamo za vitendo vya udhalilishaji wa wanawake.
Awali, kabla ya Spika kuingia bungeni kikao cha Bunge kilikuwa kikiongozwa na Mwenyekiti, Job Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa CCM, ambaye alionekana kutaka kuikubali ripoti hiyo ya Serikali kabla ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka kusimama na kueleza Bunge kuwa kwa sehemu kubwa ripoti ya Waziri Mwangunga imejaa uongo na hivyo kuomba mwongozo wa Spika ili kutoa uamuzi utakaolinda maslahi ya wananchi.
Kutokana na uamuzi huo, Ndugai alikubali na kueleza kuwa atalifikisha suala hilo kwa Spika ambaye atatoa uamuzi na ilipofika kikao cha jioni siku hiyo, Spika akatoa msimamo kuwa atatuma timu ya wabunge kwenda Loliondo, hatua ambayo bila shaka mbele ya kina Kingunge itaendelea kumtafsiri Sitta kama kikwazo kwa mambo ya serikali kupita bila kujali yana maslahi ya wananchi au la.
Ripoti ya kamati ya Mwinyi inatarajiwa kuwasilishwa katika mkutano ujao wa NEC-CCM bila shaka baada ya kupitia mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete, ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho.
Kwa muda mrefu kumekuwa na wito wa kutaka Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba aenguliwe katika wadhifa huo kutokana na tuhuma mbalimbali zikiwamo za kuendelea siasa za makundi kwenye chama hicho. Kati ya matukio yanayomuhukumu Makamba ni kitendo chake cha kumlaani kada machachari wa CCM, Nape Nnauye, aliyejitokeza hadharani na kudai kuwa mkataba wa ujenzi katika jengo la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Upanga Dar es Salaam ni wa wizi na unaonyonya jumuiya hiyo.
Katika shutuma zake hizo, Nape alitaka baadhi ya viongozi wa Baraza la Wadhamini wa UVCCM akiwamo Edward Lowassa, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kwa kashfa ya Richmond , awajibike. Makamba aliwatetea wadhamini hao akishirikiana na aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Dk. Emmanuel Nchimbi.
Hata hivyo, suala hilo lilifikishwa kwenye NEC-CCM na uamuzi ulitolewa kuwa iundwe kamati kuchunguza na ikibidi kurekebisha mkataba huo. Kamati hiyo ilifanya marekebisho makubwa, uamuzi ambao kwa namna fulani unaathiri umakini wa Makamba katika utetezi wake kwa baadhi viongozi wanaodaiwa kuwamo katika kundi lake ndani ya CCM.
Tidak ada komentar:
Posting Komentar